20 Oktoba 2025 - 14:54
“Wewe ni nani hasa?”

Khamenei: "Rais wa Marekani alisafiri hadi Palestina iliyokaliwa kwa mabavu na kutoa maneno matupu yenye kejeli ili kuwatia moyo Wazayuni waliokata tamaa."

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, amekosoa vikali matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani kuhusu Iran na eneo la Asia ya Magharibi, akisema:
"Rais wa Marekani alisafiri hadi Palestina iliyokaliwa kwa mabavu na kutoa maneno matupu yenye kejeli ili kuwatia moyo Wazayuni waliokata tamaa."

Akizungumza leo asubuhi katika kikao na mamia ya vijana wa Iran waliopata medali katika mashindano ya michezo na ya kielimu ya kimataifa, Ayatollah Khamenei aliwapongeza vijana hao kama nembo ya nguvu ya kitaifa na ushahidi wa uwezo wa vijana wa Kiirani katika kupeleka jina la Iran kileleni ulimwenguni.

Kiongozi huyo alisema: “Rais wa Marekani alijaribu kuonyesha uongo na tabia za kipuuzi ili kuwapa Wazayuni matumaini, lakini kama ana uwezo, basi aende akawatulize mamilioni ya raia wa Marekani wanaoandamana dhidi yake katika majimbo yote.”

Ayatollah Khamenei aliongeza kuwa Iran ilimpa mshituko mkubwa utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 12, ambapo makombora yaliyotengenezwa na vijana wa Kiirani yalipenya ndani kabisa ya maeneo nyeti ya adui na kuyafanya kuwa majivu.

“Makombora haya hayakunuliwa wala kukodishwa — ni matunda ya juhudi na akili ya vijana wa Kiirani,” alisema. “Wakati kijana wa Kiirani anapoingia uwanjani kwa bidii na elimu, anaweza kufanya mambo makubwa kama haya.”

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya Iran vina uwezo kamili wa kutumia tena silaha hizo wakati wowote inapohitajika.

Akijibu matamshi ya Rais wa Marekani kuhusu Iran na eneo hili, Ayatollah Khamenei alisema:
“Katika vita vya Gaza, Marekani ndiyo mshirika mkuu wa jinai za utawala wa Kizayuni, kama alivyoeleza mwenyewe kwamba ‘tulichapanya kazi pamoja na Israel Gaza.’ Silaha na mabomu yaliyomiminwa juu ya watu wasio na hatia yalitoka Marekani.”

Akimjibu zaidi Rais huyo wa Marekani aliyedai kuwa anapambana na ugaidi, Kiongozi wa Mapinduzi alisema:
“Zaidi ya watoto na wachanga elfu ishirini wameuawa Gaza — je, hao ni magaidi? Magaidi wa kweli ni Marekani, ambao waliunda kundi la Daesh (ISIS) na kulitumia kuleta machafuko katika eneo hili.”

Ayatollah Khamenei alisema kuwa vifo vya watu takribani elfu sabini katika Gaza na mauaji ya zaidi ya Wairani elfu moja katika vita vya siku 12 ni ushahidi wa asili ya kigaidi ya Marekani na Israel. “Wamewaua hata wanasayansi wetu kama Dkt. Tehranchi na Dkt. Abbasi na kujivunia mauaji hayo, lakini hawawezi kuuua sayansi,” alisisitiza.

Kiongozi wa Mapinduzi pia alimjibu Rais wa Marekani aliyedai kuwa ameharibu tasnia ya nyuklia ya Iran:
“Hilo halina maana. Wewe ni nani hasa? Nini kinachokuhusu kama Iran ina teknolojia ya nyuklia au haina? Hizi ni tabia za uonevu na uingiliaji wa mambo ya ndani ya wengine.”

Ayatollah Khamenei pia alikumbusha maandamano ya mamilioni ya Wamarekani wanaompinga Rais wao na kusema:
“Kama kweli una uwezo, tuliza hao mamilioni wanaopinga sera zako badala ya kuingilia mambo ya mataifa mengine.”

Alisisitiza kuwa Marekani ndiyo madhihirisho halisi ya ugaidi, na madai yake ya kupenda watu wa Iran ni uongo:
“Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinaumiza watu wetu moja kwa moja; kwa hivyo, Marekani ni adui wa Wairani, si rafiki.”

Kiongozi huyo aliongeza:
“Marekani inadai kupenda amani, lakini wao ndio wanaoanzisha vita. Uwepo wa kambi nyingi za kijeshi za Marekani katika eneo hili ni ushahidi wa wazi. Hii si ardhi yako; hii ni ardhi ya watu wa eneo hili.”

Akihitimisha hotuba yake, Ayatollah Khamenei alisema:
“Matamshi ya Rais wa Marekani ni ya uongo, ya kiimla, na yenye uonevu. Ingawa yanaweza kuwaathiri baadhi ya nchi dhaifu, lakini kwa neema ya Mwenyezi Mungu, hayatawahi kuwa na athari yoyote kwa taifa la Iran.”

Katika hafla hiyo, timu ya vijana wa michezo ya jadi ya Iran ilionyesha maonyesho yaliyopokelewa kwa pongezi na tabasamu la Kiongozi wa Mapinduzi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha